Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) taifa na mgombea wa nafasi ya hiyo kwenye uchaguzi unaoendelea ndani ya chama hicho, Freeman Mbowe amekacha mdahalo uliokuwa umeandaliwa na kituo cha runinga cha Star TV ambao unafanyika usiku wa leo Jijini Dar es Salaam.
Kituo cha Star TV kupitia kwa mwandaaji wa mdahalo huo Edwin Odemba amesema kwa wiki kadhaa sasa amefanya jitihada za kila aina kumtafuta Mwenyekiti Freeman Mbowe kwa ajili ya kupata uthibitisho wake kushiriki mdahalo huo pasipo mafanikio.
Hata mara baada ya kuona imekuwa ngumu kumpata Freeman Mbowe kwa ajili ya kuthibitisha kushiriki mdahalo huo, Odemba aliamua kumtafuta Katibu Mkuu wa chama hicho John Mnyika kwa ajili ya kusaidia kumpata Mwenyekiti Mbowe ili athibitishe kuhudhuria mdahalo, hata hivyo Mnyika amesisitiza kuwa suala la mdahalo ni la mgombea binafsi, hivyo waandaaji wamtafute Freeman Mbowe mwenyewe.
Taarifa za kuaminika kutoka kwa wandani wa Freeman Mbowe zinaeleza kuwa Mbowe amekacha mdahalo huo kwa kile anachoamini kuwa kufanya hivyo ni ‘kubagaza’ chama.
Mgombea Tundu Lissu kupitia ukurasa wake wa X amethibitisha kushiriki mdahalo huo na amesema mdahalo kwa wagombea ni utamaduni wa kisiasa unaopaswa kujengwa na kukuzwa kama sehemu ya ujenzi wa demokrasia nchini Tanzania.
Kwa upande wake mgombea Odero Charles Odero ameiambia Jambo TV kuwa atashiriki mdahalo huo, na hakika Jambo Tv tutakuletea mdahao huo mbashara.