Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (@chadematzofficial ), @freemanmbowetz, amefanya mahojiano maalum na wahariri pamoja na waandishi wa habari kutoka kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) jijini Dar es Salaam, jana Januari 17, 2025, ambapo amezungumzia hali ya chama, mchango wa @godbless_lema katika siasa za CHADEMA na nafasi ya kada huyo ambaye alikuwa ni mbunge wa jimbo la Arusha Mjini.
Mbowe amesema kuwa, licha ya mchango mkubwa aliowahi kutoa Lema, kwa sasa hana mamlaka yoyote ndani ya chama na kwamba amebaki kuwa tu mwanachama wa kawaida.
Kwa mujibu wa katiba ya CHADEMA, mamlaka ya kinidhamu kwa mwanachama wa kawaida yapo katika ngazi ya tawi, hali inayomaanisha kuwa hata tawi linaweza kumfukuza uanachama.
Mbowe amesisitiza kuwa, siasa ni mchezo wa pamoja na hakuna mtu au kikundi cha watu mmoja kujiona wana umuhimu kuliko chama na kwamba bila wao chama hakiwezi kwenda.
“Leo unaweza kuwa mashuhuri, kesho hautakuwa mashuhuri. Nani alikuwa mashuhuri kama marehemu Augustino Mrema, nani alikuwa mashuhuri kama Zitto Kabwe enzi zake, bado ni kijana kuliko mimi, lakini kisisas yuko wapi? Siasa ni mchezo wa pamoja na tunahitajiana” alisema Mbowe, akionesha kuwa CHADEMA ina uwezo wa kusimama hata bila wanachama maarufu.
Mbowe ameweka wazi kwamba, Lema alikuwa na vipaji vyake na uwezo mkubwa, lakini alikabiliwa na changamoto kubwa za uongozi wakati alipokuwa Mwenyekiti wa Kanda ya Kaskazini.
Amedai kuwa Lema hakufanikiwa kuunda hata kamati za uongozi wa kanda katika kipindi cha miaka mitano, jambo lililosababisha migogoro mingi ndani ya kanda hiyo.
“Waliomkataa Lema siyo mimi, bali ni viongozi wa mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Tanga, na Manyara. Miaka mitano ya uongozi wake ilikuwa na migogoro mingi,” alisema Mbowe.
Aidha, Mbowe amesisitiza kuwa, Lema alipokuwa katika uongozi alishindwa kutumia nafasi yake kutatua changamoto za kanda hiyo na kwamba hata alipokuwa uhamishoni, bado alipaswa kushirikiana na viongozi kufanya vikao vya uongozi.
Mbowe ameonesha kushangazwa na ukosoaji wa Lema kwa uongozi wa chama kwa sasa, akisema kuwa alikuwa na nafasi ya kuleta mabadiliko alipokuwa Mjumbe wa Kamati Kuu.