UONGOZI wa Kagera Sugar upo katika mazungumzo ya kupata saini ya nyota wa Yanga, Denis Nkane kwa mkopo wa miezi sita ukiwa na imani anaweza kukisaidia kikosi cha timu hiyo.
Taarifa kutoka Kagera Sugar zinasema kuwa tayari wameshaiandikia barua Yanga kumuomba mchezaji huyo ambaye chini ya kocha Sead Ramovic hajapata nafasi ya kucheza mechi hata moja kati ya tisa alizosimamia Mjerumani huyo.
“Tunasubiri majibu kutoka Yanga, lakini hiyo ofa tayari tumeshaituma na tunaaamini kama tutampata mchezaji huyo ataongeza kitu ndani ya timu yetu ambayo haijawa na mwanzo mzuri mzunguko wa kwanza wa ligi, hivyo dirisha hili tunahitaji kujiimarisha,” kilisema chanzo chetu.
“Nkane akipatikana ataingia moja kwa moja kikosi cha kwanza kutokana na uwezo alionao. Sio kila mchezaji ambaye hapati nafasi ya kucheza timu kubwa za Simba na Yanga hana uwezo, wana uwezo mkubwa shida ni kukosa nafasi, hivyo tunaamini akija Kagera Sugar ataingia moja kwa moja kikosini.”
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Kagera Sugar, Thabiti Kandoro alisema hawezi kuzungumzia suala la mchezaji huyo, ingawa kama viongozi walishaanza taratibu za kukamilisha baadhi ya usajili wa wachezaji kutokana na mapendekezo ya benchi la ufundi.
“Ni kweli suala hilo lipo lakini hatuwezi kulizungumzia kwa sababu mchakato bado haujakamilika. Mambo yakienda kama yalivyopangwa taarifa itatolewa. Kwa sasa tunaomba tuliache,” alisema Kandoro.
Nkane aliyejiunga na Yanga katika dirisha dogo la Januari 2021 akitokea Biashara United ya Mara, ameshindwa kuingia moja kwa moja kwenye kikosi cha kwanza kutokana na ushindani uliopo chini ya makocha watatu akianza Nasreddine Nabi, Miguel Gamondi na sasa Sead Ramovic.