MKURUGENZI Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk. Anna Henga, amesema kinachoendelea katika Chama cha Demokrasia na Maendeelo (CHADEMA), ni ishara tosha kwamba demokrasia bado ina shida nchini.
Amesema tatizo hilo pia haliko kwa chama hicho pekee bali hata Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwenye baadhi ya uchaguzi wake wa ndani huwa kunaibuka mijadala inayofafania na kinachoendelea CHADEMA.
Alisema hayo jana jijini Dar es Salaam alipozungumza na Nipashe, akieleza kuwa tuhuma za rushwa ndani ya CHADEMA zinaweza kuwa za kweli au zina nia ya kumchafua mtu. Ukweli wake unaweza kuthibitika mahakamani.
"Mchakato wa kidemokrasia hapa nchini una shida, si tu kwa CCM wala CHADEMA, angalau kidogo kwa Chama cha ACT-Wazalendo huwa wanajitahidi kujiepusha na kama huwa yanatokea wana namna ya kudhibiti," alisema Dk. Anna ambaye kitaaluma ni mwanasheria.
Alisema demokrasia nchini bado ni changa na hakuna mipango ya kuifanya ikomae, huku akisisitiza suluhu ya yote hayo ni Katiba mpya.
"Tungeweza kuwa na Katiba mpya ambayo inatoa mwongozo wa kidemokrasia, Tume Huru ya Taifa Uchaguzi (INEC), ingekuwa na mwongozo ambao na wengine wangefuata. Ninadhani ingekuwa suluhu kwa ukuzaji wa demokrasia nchini.
"Ukiona mzazi ana changamoto basi hata watoto lazima watakuwa nayo, pia katika uchaguzi wa CHADEMA, nimeona wanaume wengi wamechaguliwa katika nafasi mbalimbali. Hii inaonesha nafasi ya wanawake ndani ya chama hicho bado ni ndogo," alisema Dk. Anna.
Alishauri kuwe na mabadiliko makubwa ya kisheria ili kuwa na demokrasia katika uchaguzi japo ni ngumu kwa sasa kwa sababu vitu vingi vimo katika Katiba.