Huduma za TikTok zimeanza tena kutolewa kwa watumiaji wake milioni 170 nchini Marekani baada ya Rais Mteule Donald Trump kuahidi kusitisha utekelezaji wa sheria ya kuipiga marufuku programu hiyo. Hatua hiyo imechukuliwa mara baada ya Trump kusema atatoa nafasi kwa majadiliano yatakayopelekea suluhisho la kudumu kuhusu matumizi ya programu hiyo inayomilikiwa na kampuni ya Kichina.
TikTok ilikuwa imesitisha huduma zake Jumamosi jioni kwa watumiaji wake nchini Marekani kufuatia kuanza kutekelezwa kwa sheria iliyokuwa imeipiga marufuku kwa sababu za kiusalama. Serikali ya Marekani awali ilikuwa imeeleza hofu kwamba data za watumiaji wa TikTok zinaweza kufikia serikali ya China, jambo ambalo liliibua wasiwasi wa usalama wa taifa.
Jumapili, Rais Mteule Trump, ambaye hapo awali aliunga mkono marufuku hiyo, alitangaza kusitishwa kwa muda utekelezaji wa sheria hiyo ili kutoa nafasi kwa mazungumzo na kutafuta suluhisho bora.
"Tunahitaji kuhakikisha usalama wa taifa letu, lakini pia ni muhimu kutoa nafasi ya majadiliano na maelewano," amesema Trump.
TikTok imetoa taarifa mara baada ya kurejesha huduma zake, ikielezea shukrani zake kwa Trump kwa kutoa uhakikisho wa kuwepo nafasi ya mazungumzo.
"Tunamshukuru Rais Mteule Trump kwa kutoa uhakikisho unaohitajika. Tutashirikiana naye na timu yake ili kutafuta suluhisho la kudumu ambalo litaruhusu TikTok kuendelea kutoa huduma zake nchini Marekani," imesema kampuni hiyo.
Watumiaji wa TikTok wameonesha shukrani zao kupitia jukwaa hilo, wakieleza furaha yao kwa kurejeshwa kwa huduma za programu hiyo maarufu ya mitandao ya kijamii.
TikTok sasa inatarajiwa kushirikiana na timu ya Trump kufikia makubaliano ya kudumu, ambayo yatalinda data za watumiaji wa Marekani huku ikiruhusu programu hiyo kuendelea kufanya kazi.