Rais wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS), Wakili Boniface Mwabukusi amesema angekuwa mpiga kura wa uchaguzi wa taifa ndani ya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) @chadematzofficial angemchagua Tundu Lissu kwa sababu ni kiongozi mzalendo, jasiri na muwazi kwa maslahi ya umma.
Wakili Mwabukusi amesema wanachama wa CHADEMA ndio wanajua aina ya kiongozi wanayemtaka lakini kwa maoni yake angekuwa mpiga kura angemchagua Tundu Antipas Lissu ili aendeleze alipoishia mtangulizi wake (Freeman Mbowe).
"Mimi nadhani wenye uwezo wa kuamua nani atafaa ni wanaChadema lakini nawatahadharisha kwamba Watanzania wana akili wanaona na wanajua nani anaweza kuwatoa hapa walipo lakini ungeniambia Mwabukusi kapige kura basi ningempigia Tundu Lissu na nina sababu za kwangu kumpigia Lissu, simpigii kura Lissu kwa sababu ni malaika lakini nampigia kwa sababu nafikiri is a right person who can take this new challenges (ni mtu ambaye anaweza kuzichukulia changamoto mpya za chama) na sio kwamba yeye ni malaika asilimia mia moja hapana hakuna mtu mtu aliyekamilika kila mtu ana changamoto zake uzuri na uzuri na kwenye udhaifu ndipo tutakapoimarishana," amesema Wakili Mwabukusi.
Baada ya kuulizwa sababu za kudhani Lissu anafaa kuwa mwenyekiti wa CHADEMA, wakili Mwabukusi amejibu kuwa.
"Lissu ni mkweli, Lissu ni muwazi, mahali pa kukukemea atakukemea na mahali pa kukupongeza atakupongeza, ni mtu anayetetea kile anachokiamini, Lissu anaamini katika katiba mpya, Lissu anaamini katika utawala bora, Lissu anaamini katika ulinzi na utetezi wa raslimali za Taifa na haki za binadamu, kuna watu wanahoji kuwa Lissu ni mkali hapana tutamwambia akiwa mkali panapotakiwa kuwa mpole, hatutashindwa kumwambia kama tunavyomwambia Mbowe pumzika," amesema Mwabukusi.
Hata hivyo kuhusu usiri kwa Lissu, Mwabukusi ameeleza kuwa "Mimi nashangaa mtu anayesema Lissu hana busara, kwanza kipimo cha busara kiko wapi na anayepima busara ni nani, huo ni ujinga tu hakuna busara zinazoweza kushindana na ukweli, kama tuna uwezo wa kuikosoa Serikali kwa nini hatuwezi kujikosoa masuala ya rushwa akikemea nje ya chama kuna shida gani kama ndani hasikilizwi," ameeleza Mwabukusi.