Mzee Magoma, mmoja wa wanachama wa muda mrefu wa Yanga SC, amezua gumzo kubwa baada ya kufichua masuala mazito yanayoikumba klabu hiyo.
Kulingana Na EASTAFRICA tv,akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Mzee Magoma alimtaja bila uoga kiongozi anayehusishwa na vurugu za kiutendaji ndani ya klabu hiyo, akidai kuwa hatua zake zinaathiri maendeleo ya timu.
Kwa mujibu wa Mzee Magoma, kiongozi huyo anadaiwa kuingilia maamuzi ya kiufundi na kiutawala, jambo ambalo limewafanya baadhi ya viongozi na benchi la ufundi kushindwa kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.
"Klabu yetu ni kubwa, lakini watu wachache wanahujumu juhudi za kuleta maendeleo. Lazima wanachama na wapenzi wa Yanga tuamke," alisema kwa msisitizo.
Akiendelea kufafanua, Mzee Magoma alidai kuwa hali hiyo imekuwa ikichangia migogoro ya mara kwa mara ndani ya timu, huku akihimiza wanachama kuchukua hatua za haraka kuhakikisha klabu inarejea kwenye mstari wa mafanikio.
"Hatuhitaji migogoro, tunahitaji mshikamano. Kiongozi yeyote anayewavuruga Yanga hana nafasi," aliongeza.
Kauli zake zimezua mjadala mkubwa kwenye mitandao ya kijamii, ambapo mashabiki na wanachama wanazidi kuhoji kuhusu utendaji wa viongozi wa klabu hiyo.
Hata hivyo, hakumtaja moja kwa moja jina la kiongozi huyo, lakini alihimiza wanachama kuangalia kwa makini mwenendo wa viongozi na kudai uwajibikaji wa dhati.
“Hii ni klabu yetu, hatuwezi kuruhusu itawaliwe na maslahi binafsi ya wachache. Lazima tuisimamie ipasavyo,” alihitimisha Mzee Magoma.
Yanga SC bado haijatoa tamko rasmi kuhusu tuhuma hizi.