Mwanza. Wanaume wawili wanaosadikiwa kuwa majambazi wenye silaha wameuawa kwa kupigwa risasi na askari wa Jeshi la Polisi mkoani Mwanza, baada ya kudaiwa kujaribu kutekeleza tukio la ujambazi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbrod Mutafungwa akizungumza na waandishi wa habari leo Ijumaa Januari 10, 2025 amesema wanaume hao ambao walivaa magauni na vilemba kuficha utambulisho wao, wameuawa usiku wa kuamkia leo.
Amesema wakiwa wanne walifika yalipo makazi ya mfanyabiashara, Flora Abdallah (42) yaliyopo Mtaa wa Kabambo, Kata ya Kiseke wilayani Ilemela, mkoani Mwanza kisha kujaribu kuingia ndani kwa ajili ya kupora fedha.
“Wanaume hao walikuwa wamevaa magauni na vilemba ili wasibainike kwa urahisi. Kwa hiyo, alipofunguliwa geti tu akiwa ndani ya gari lake, ghafla waliingia getini ndipo mfanyabiashara huyo alipokimbilia ndani,” amesema.
“Wengine wawili waliokuwa nje (majina hayajatambulika) walipobaini kuwa maofisa wetu wameshafika eneo la tukio waliwasha pikipiki yao na kutokomea kusikojulikana msako kuwatafuta unaendelea,” amesema.