Ng'ombe 16 waliokutwa wamefariki kwa kupigwa na radi katika hifadhi asilia ya Kalambo mkoani Rukwa. Picha na Neema Mtuka
Rukwa. Radi imeua ng’ombe 16 katika Kijiji cha Ngolotwa, wilayani Kalambo, mkoani Rukwa.
Tukio hilo limetokea Jumatano Januari 1, 2025 wakati ng’ombe hao wakichungwa katika hifadhi ya Kalambo mkoani humo, huku mmiliki mpaka sasa akiwa hajafahamika.
Mhifadhi Mkuu wa Wilaya ya Kalambo, Ibrahim Mkiwa amesema wamewakuta ng’ombe hao wamekufa hifadhini humo, huku akitoa rai kwa wananchi kutoingiza mifugo hifadhini.
"Ni marufuku kwa wafugaji kuchunga mifugo yao katika hifadhi sio hii tu hapa hata hifadhi nyingine kwani kwa kufanya hivyo wanaharibu na kupoteza uzuri wa hifadhi hizo ambazo zimehifadhiwa kwa lengo la kutunza uasili wake" amesema Mkiwa.
Mkiwa amebainisha kuwa kwa mfugaji atakayebainika kuingiza mifugo kwenye hifadhi atachukuliwa hatua kali za kisheria na kuitaka jamii kuwa sehemu ya kutunza na kulinda uoto wa asilia kwa kuacha kukata miti kiholela.
Mganga Mkuu wa mifugo wilayani humo, Dk Ennosy Luvinga amesema baada ya uchunguzi wamebaini ng’ombe hao wamekufa kwa kupigwa na radi.
Hili ni tukio la pili mfululizo kwa mifugo kufa kwa kupigwa na radi mkoani humo, ambapo la kwanza lilitokea Desemba 9, 2024 baada ya ng'ombe 22 kupigwa radi wakiwa zizini katika Kijiji cha Songambele Kata ya Azimio wilayani Sumbawanga.
Mmoja wa wananchi Edson Juakali amesema kuwa ukosefu wa maeneo ya kuchungia mifugo ndio sababu ya wafugaji kuingiza mifugo yao katika hifadhi ili wapate malisho.
"Tunaiomba serikali iwatengee maeneo ya kuchungia mifugo ili wasiendelee kuleta madhara kwani huingiza mifugo hata kwenye mashamba jambo ambalo huchochea vurugu"
Kwa upande wake Ofiisa Misitu wa Halmashauri ya Wilaya ya Kalambo, Geofrey Mwasomola ametumia fursa hiyo kuwataka wafugaji kuwa sehemu ya kutunza na kulinda mazingira kwa kuwa na maeneo ya kutosha kwa ajili ya ufugaji kama sheria inavyotaka.