Rais wa TLS Ahoji Wachezaji wa Singida Black Stars Kupewa Uraia




Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Boniface Mwabukusu, ameibua maswali mazito kuhusu mchakato wa kupewa uraia wa Tanzania wachezaji watatu wa timu ya mpira wa miguu ya Singida Black Stars.

Maswali haya yanakuja baada ya Idara ya Uhamiaji kutoa taarifa ikithibitisha kuwa Emmanuel Kwame Keyekeh (Ghana), Josephat Arthur Bada (Cote d'Ivoire), na Muhamed Damaro Camara (Guinea) wamepewa uraia kwa mujibu wa Sheria ya Uraia ya Tanzania, Sura ya 357.

Katika taarifa yake, Mwabukusu amesema, “Sasa kwa nini tunakataa uraia pacha kama uraia unaweza kugawiwa kwa wageni kwa urahisi namna hii?”

Aliongeza kuwa sheria ya uraia inahitaji mgeni aishi Tanzania kwa kipindi kisichopungua miaka 10 kabla ya kuomba uraia, isipokuwa katika mazingira maalum kama uraia wa heshima, ndoa, au maslahi ya kitaifa.

Mwabukusu amehoji iwapo wachezaji hao wanatimiza vigezo hivyo maalum.




“Waziri mwenye dhamana atoke na kutueleza kwa kutoa ufafanuzi wa kina unaoeleweka. Hatupingi watu kupewa uraia, lakini uraia haupewi kama karanga za kuonjeshwa. Lazima kuzingatia sheria na taratibu,” alisema.

Kauli hii imeibua mijadala mitandaoni, huku baadhi ya wananchi wakitaka uwazi zaidi juu ya mchakato wa utoaji wa uraia nchini.

Idara ya Uhamiaji, kupitia taarifa yake, imesisitiza kuwa wachezaji hao walipata uraia kwa kufuata sheria, lakini haikutoa maelezo ya kina kuhusu vigezo walivyotimiza.

Wananchi na viongozi wa kisheria sasa wanasubiri majibu kutoka kwa Waziri wa Mambo ya Ndani ili kufafanua zaidi kuhusu suala hili.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad