Shirika la Reli Tanzania (TRC), limetoa pole na kuwaomba radhi abiria waliokuwa wakisafiri kati ya Dar es Salaam, Morogoro na Dodoma Januari 08, 2025 kufuatia usumbufu uliojitokeza kutokana na hitilafu ya kiufundi iliyotokea katika kituo cha lhumwa Dodoma majira ya saa 5:38 usiku ambapo limesema linajua safari za kawaida kati ya Dar es salaam na Dodoma zimeathirika na hii inaweza kuwa na athari kubwa kwa abiria.
Taarifa iliyotolewa na TRC usiku huu imesema Mafundi wa Shirika hilo wamepambana kurekebisha tatizo husika na kuhakikisha huduma zake zinarejea kwenye hali ya kawaida huku ikibainisha kuwa treni zilizoathirika ni treni iliyoondoka saa 12.55 jioni siku ya Jumanne Januari 7, 2025 kutoka Dar es salaam kuelekea Dodoma iliyotarajiwa kufika 5.01 usiku badala yake ilifika saa 7 usiku.
“Treni nyingine ni ile inayoondoka saa 11.15 asubuhi siku ya Jumatano Januari 8, 2025 kutoka Dodoma kuelekea Dar es salaam iliondoka saa 3.05 asubuhi, treni iliyotakiwa kuondoka saa 12.00 asubuhi Januari 8, 2025 kutoka Dar es Salaam kueleka Dodoma iliondoka saa 12.30 asubuhi na treni iliyotakiwa kuondoka saa 3.30 asubuhi siku ya Jumatano Januari 8, 2025 imeondoka saa 11.55 kutoka Dar es Salaam Kuelekea Dodoma” ——imesema taarifa ya TRC.