Jeshi la Polisi Tanzania limesema linamsaka Kijana mmoja ambaye amejirekodi video na kuisambaza mtandaoni akitangaza kuwa anamuuza Mtoto aliyembeba kwa shilingi milioni moja na laki sita.
Taarifa iliyotolewa leo January 03,2025 na Msemaji wa Jeshi la Polisi imenukuliwa ikieleza yafuatayo “Jeshi la Polisi linamtafuta kwa kuendesha msako Nchi nzima Mtu ambaye anaonekana ametengeneza picha mjongeo ( video clip) akitangaza kuwa anamuuza Mtoto aliyembeba kwa shilingi milioni moja na laki sita, msako huo utahakikisha anakamatwa ili hatua nyingine za kisheria ziweze kufuata”
“Aidha, Jeshi la Polisi linalaani kitendo hicho cha kikatili na kilicho kinyume na sheria, pia linatoa wito kwa Wananchi kuendelea kufichua vitendo kama hivyo, kuvilaani na kuvikemea kwani vinaweza kusababisha madhara kwa Watoto ili hatua zichukuliwe kabla madhara hayajatokea” - imeeleza taarifa ya Polisi.
Hata hivyo saa zaidi ya 23 zilizopita Kijana huyo alijirekodi video nyingine akisema nia yake haikuwa kumuuza Mtoto huyo bali alikua akitengeneza tu maudhui ya mtandaoni “Jamani Watanzania nimekuja mbele yenu, huyu ni Mtoto wa Dada yangu naona wengi mmecomment sana, mimi huyu Mtoto ni damu yangu, nilichokuwa nakifanya jana ilikua ni ‘content’ kwahiyo mnaonihisi vibaya mimi siko huko, naomba mnisamehe kwa wale niliowakwaza”