Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa tahadhari kuhusu vipindi vya mvua kubwa vinavyotarajiwa katika baadhi ya maeneo nchini.
Kanda za Ziwa Victoria, ikijumuisha mikoa ya Kagera, Geita, Shinyanga, Mwanza, Simiyu, na Mara, zinatarajiwa kushuhudia mvua zitakazoambatana na ngurumo za radi katika maeneo machache.
Hali kama hiyo pia inatarajiwa katika Nyanda za Juu Kaskazini Mashariki, hususan mikoa ya Arusha, Manyara, na Kilimanjaro, kuanzia kesho jioni.
Katika Pwani ya Kaskazini, mikoa ya Tanga, Pwani, na Dar es Salaam, pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba, mvua zitakazoambatana na ngurumo za radi zinatarajiwa.
Maeneo ya kaskazini mwa Morogoro nayo hayatabaki nyuma katika kushuhudia mvua hizi.
Kwa upande wa Magharibi mwa nchi, mikoa ya Kigoma, Katavi, na Tabora inatarajiwa kuwa na vipindi vya mvua za radi katika maeneo machache.
Aidha, mikoa ya Dodoma na Singida katika Kanda ya Kati itapata vipindi vya mvua nyepesi kwa kiasi kidogo.
Nyanda za Juu Kusini Magharibi, ikijumuisha mikoa ya Rukwa, Songwe, Mbeya, Njombe, na Iringa, inatarajiwa kushuhudia vipindi vya mvua nyingi.
TMA imehimiza tahadhari, ikionya kuwa mvua hizi zinaweza kusababisha madhara, ikiwemo mafuriko, uharibifu wa miundombinu, na athari kwa shughuli za kijamii na kiuchumi.
Wananchi wanashauriwa kufuatilia taarifa za hali ya hewa mara kwa mara na kuchukua tahadhari stahiki.