“Kuanzia sasa kama tutashiriki tena kwenye chaguzi zijazo ukiwemo uchaguzi mkuu 2025 bila kuwa na Katiba mpya na mfumo mpya wa kidemokrasia wenye Tume huru ya uchaguzi na sheria mpya za uchaguzi tutashiriki huku tukijua kwamba Wapiga kura feki wataandikishwa, Wagombea wetu wataenguliwa, tutafanyiwa vurugu kwenye kampeni na siku ya uchaguzi, kura feki zitaingizwa na kura halali zitaibiwa, na Wagombea walioshindwa watatangazwa Washindi wa chaguzi hizo”
“Ukweli huu mchungu unatutaka tubadilishe mbinu za mapambano ya kidemokrasia, tumesubiri CCM na Serikali zake wabadilishe msimamo wao kuhusu Katiba mpya na Tume huru kwa miaka mingi, tumewabembeleza kwa muda mrefu wakubali Nchi yetu iondokane na Katiba ya sasa bila mafanikio”
“Kuhusu uchaguzi wa Chama chetu, Mwenyekiti wetu wa Chama na Mgombea mwenzangu wa Uenyekiti wa CHADEMA (Freeman Mbowe) amesema uchaguzi wetu wa Chama unatakiwa kuwa huru na haki nami naunga mkono maneno yake, bila uchaguzi huru Wanachama wetu hawatopata fursa ya kuonesha kuwa wao ndio wenye madaraka ya mwanzo na mwisho katika kuamua hatima ya Chama chetu, ili haya yatekelezwe tunahitaji kutafakari masuala yafuatayo”
“Napendekeza kuwa pamoja na Wazee Wastaafu wa Chama watakaopatikana kusimamia uchaguzi, Kamati Kuu iwaombe Viongozi wa Dini kuhudhuria mkutano mkuu kama Watazamaji ili kusaidia kuzuia mipango ya Waovu kuvuruga uchaguzi wetu, Kamati Kuu pia iwaite Wawakilishi wa Balozi mbalimbali nchini kushuhudia uchaguzi wetu” —— Mgombea wa Uenyekiti wa CHADEMA Taifa, Tundu Lissu akiongea na Watanzania leo January 01,2025