Ahoua, Kibu walivyobeba matumaini ya Simba CAF
Alhamisi, Januari 09, 2025Kiungo wa Simba, Jean Charles Ahoua mpaka sasa ndiye mchezaji aliyehusika kwenye mabao mengi ndani ya Simba katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika na Ligi Kuu Bara.
Mchango huo wa mabao umeifanya Simba kuongoza msimamo wa Ligi Kuu Bara na kujiweka pazuri kwenye kufuzu robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Nyota huyo raia wa Ivory Coast, alitua Msimbazi msimu huu akitokea Stella Club d'Adjamé ya nchini kwao ambako alifanya vizuri msimu uliopita na kuwa mchezaji bora wa Ligi Kuu (MVP) msimu wa 2023-2024 ambapo alifunga mabao 12 na kutoa pasi tisa za mwisho.
Baada ya kuhamia Simba, Ahoua ameendeleza kile alichokuwa akikifanya Ivory Coast huku akiwa miongoni mwa nyota waliobeba matumaini ya timu hiyo katika kufuzu robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Kwenye mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika hatua ya makundi, nyota huyo amecheza michezo yote minne kwa dakika 319, akifunga mabao mawili kati ya matano ambayo Simba imefunga na kutoa pasi mbili za mabao.
Wakati Ahoua akifanya hivyo, Kibu Denis anafuatia kwa kufunga mabao mawili, lingine mfungaji ni nahodha, Mohamed Hussein 'Tshabalala'.
Mchezo wa kwanza wa makundi uliopigwa uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam, Ahoua alifunga bao pekee dakika ya 34 katika ushindi wa 1-0 dhidi ya Bravos.
Katika mchezo wa pili uliopigwa Algeria kwenye Dimba la Chahid Hamlaoui, wakati Simba ikifungwa 2-1 na CS Constantine, Mohamed Hussein 'Tshabalala' ndiye aliifungia Simba dakika ya 24 kwa pasi ya Ahoua.
Baada ya kutoka Algeria, Simba ilirudi nyumbani kucheza mchezo wa tatu dhidi ya CS Sfaxien ya Tunisia ambapo iliibuka na ushindi wa mabao 2-1 ikitoka nyuma baada ya wageni kufunga kupitia Haj Hassen dakika ya tatu kabla ya Kibu Denis kusawazisha dakika ya saba akipewa pasi na Ahoua wakati bao la pili likifungwa tena na Kibu dakika ya 90+8.
Mchezo wa nne Simba ilicheza Januari 5, 2025 ikirudiana na Sfaxien ambapo ilipata ushindi wa bao 1-0 lililofungwa na Ahoua dakika ya 34 na kuifanya Simba kupata ushindi wa kwanza Ukanda wa Kaskazini mwa Afrika tangu ilipofanya hivyo mwaka 2003 dhidi ya Zamalek ya Misri.
Simba inashika nafasi ya pili kwenye kundi A la michuano hiyo ikiwa na pointi tisa sawa na CS Constantine inayoongoza kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa. Nafasi ya tatu inashikwa na Bravos yenye pointi sita wakati Sfaxien inaburuza mkia ikiwa haina pointi baada ya kuambulia vipigo katika mechi zote nne.
Zimebaki mechi mbili kwa Simba kuifukuzia rekodi ya kufuzu robo fainali ya michuano ya Caf kwa mara ya sita ndani ya misimu saba kuanzia 2018-2019 huku pia ikiwa ni mara ya pili ndani ya Kombe la Shirikisho Afrika kwa kipindi hicho.
Katika robo fainali tano zilizopita, nne za Ligi ya Mabingwa msimu wa 2018-2019, 2020-2021, 2022-2023 na 2023-2024 wakati 2021–22 ikiwa ni Kombe la Shirikisho.
Ligi Kuu napo hakujapoa
Katika mechi 15 za Simba ikiwa imefunga mabao 31, Ahoua amehusika katika mabao 12 akifunga saba na kutoa pasi tano za mwisho huku akiwa ndiye kinara wa mabao na asisti ndani ya kikosi cha Simba. Kwa mabao kikosini hapo anafuatia mshambuliaji, Leonel Ateba mwenye matano huku Steven Mukwala akiwa nayo manne.
Mabao waliofunga nyota hawa unaifanya Simba kushika nafasi ya kwanza kwenye Ligi Kuu ikiwa na pointi 40 mbele ya watani zao Yanga walio nafasi ya pili na pointi 39.
Ukiachana na wachezaji hao yupo golikipa, Moussa Camara ambaye amefanikiwa kulinda vizuri lango la Simba akiwa ameruhusu mabao matano kuingia wavuni huku akiongoza ‘Clean sheet’ akiwa nazo 12 akiwaacha Patrick Munthar wa Mashujaa mwenye ‘Clean sheet’ nane wakati Djigui Diarra (Yanga) na Metacha Mnata (Singida Black Stars) wakiwa nazo saba kila mmoja.