Wasifu wa Dkt. Tulia Ackson, Elimu, Umri, Familia na Mengineyo



Dkt. Tulia Ackson alizaliwa tarehe 23 Novemba 1976 katika Kata ya Bulyaga, Tukuyu, Wilaya ya Rungwe, Mkoa wa Mbeya. Alianza safari yake ya elimu katika Shule ya Msingi Mabonde, Tukuyu (1984-1990), kisha akaendelea na masomo ya sekondari katika Shule ya Wasichana ya Loleza, Mbeya (1991-1994) na Shule ya Wasichana ya Zanaki, Dar es Salaam (1995-1997).

Mwaka 1998, alijiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na kufuzu Shahada ya Sheria (LL.B) mwaka 2001, na Shahada ya Uzamili ya Sheria (LL.M) mwaka 2003. Aliendelea na masomo katika Chuo Kikuu cha Cape Town, Afrika Kusini, ambako alipata Shahada ya Uzamivu (PhD) katika Sheria mwaka 2007.


Alianza kazi ya kufundisha katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mwaka 2001 kama Msaidizi wa Kufundisha na kufikia ngazi ya Mhadhiri Mwandamizi mwaka 2011. Aidha, alihudumu kama Naibu Mkuu wa Kitivo cha Sheria kati ya mwaka 2009 na 2015.

Mwaka 2014, Rais Jakaya Kikwete alimteua Dkt. Tulia kuwa mjumbe wa Bunge Maalum la Katiba akiwakilisha taasisi za elimu ya juu. Mwaka 2015, alihudumu kwa muda mfupi kama Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali kabla ya kuteuliwa kuwa Mbunge na Rais John Magufuli. Baada ya hapo, alichaguliwa kuwa Naibu Spika wa Bunge.

Katika uchaguzi wa mwaka 2020, Dkt. Tulia alichaguliwa kuwa Mbunge wa Jimbo la Mbeya Mjini na akarejea nafasi ya Naibu Spika. Tarehe 1 Februari 2022, alichaguliwa kuwa Spika wa Bunge, akiwa mwanamke wa pili kushika wadhifa huo nchini Tanzania.

Kwa ngazi ya kimataifa, tarehe 27 Oktoba 2023, alichaguliwa kuwa Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) katika mkutano wake wa 147 huko Luanda, Angola, akiwa Mtanzania wa kwanza kushika nafasi hiyo.

Dkt. Tulia ni mke na mama wa watoto wawili. Anaongea Kiswahili, Kiingereza, na Kifaransa. Anapenda sana ngoma za kitamaduni, kushiriki mbio za marathon, na kucheza netiboli.

Mwaka 2015, alianzisha taasisi ya Tulia Trust, ambayo inalenga kuwasaidia makundi yenye mahitaji maalum nchini Tanzania. Shughuli za taasisi hiyo zinahusisha kukuza elimu ya wasichana, kuwawezesha kiuchumi jamii za vijijini, na kuboresha huduma za afya ya mama.


Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad