Waziri wa Maendeleo ya Jamii Jinsia na Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Dorothy Gwajima ameliamuru jeshi la polisi limtafute na kumkamata kijana aliyetangaza mtandaoni kuwa anauza figo za mtoto wake.
…
Kupitia mtandao wa TikTok, mtengeneza maudhui anayefahamika kama Jideboy alitangaza kuwa tajiri yoyote apeleke kwake Tsh. milioni 1.6 kwani mtoto aliyembeba ana figo 2.
…
“Baadhi ya Content Creators kama Jideboy mmefikia hatua mbaya. Nakemea vikali. Tayari nimewakabidhi polisi wamtafute huyu. Watanzania tusaidiane kumjua huyu ni nani na wapi alipo,” ameandika Waziri Gwajima kupitia ukurasa wake wa mtandao wa X.
“Huwezi kutania jambo kama hilo huku walaji wa utani wako wakiwa ni mamilioni ya Watanzania wenye akili mbalimbali. Unadhalilisha mtoto kwa jila la utani na kumweka hatarini. Unajua kwa sasa kuna tatizo la usafirishaji haramu wa watoto,? Gwajima amemjibu mtumiaji wa mtandao wa X ambaye alidai kuwa huenda Jideboy alikuwa anatania.
…
Baada ya watu wengi kumsema vibaya kutokana na nia yake hiyo ya kutaka kuuza viungo vya binadamu, kijana Jideboy amechapisha video nyingine akiomba msahama.
“Naombeni mnisikilize kwa makini. Huyu mtoto ni mjomba wangu, mtoto wa dada yangu. Naona wengi mme-comment sana kwamba naweza kuwa muuaji. Niwaambike kitu, huyu ni damu yangu. Nilichokuwa nakifanya jana ni content tu. Naomba mnisamehe kwa wale ambao nitakuwa nimewakwaza. Kuna baadhi ya watu hawana watoto,” amesema Jideboy kupitia ukurasa wake wa Tiktok.
Wadau wengi wameungana na Waziri Gwajima kukemea matukio kama hayo huku wakitaka adhabu kali itolewe kwa kijana huyo ili liwe fundisho kwa watengeneza maudhui wengine.