Klabu hiyo inasema kuwa usajili huu utahusu mchezaji ambaye atakuwa gumzo kwenye dirisha dogo la usajili, huku taarifa zikisema kuwa Yanga imeingilia kati dili la Simba kumtaka straika anayeongoza kwa mabao kwenye Ligi Kuu, Elvis Rupia
Awali, Simba ilijulikana kuwa na mazungumzo ya kumtua Rupia, mshambuliaji kutoka Kenya anayekipiga kwa Singida Black Stars.
Hata hivyo, Yanga imeingilia kati na inaelekea kumaliza mchakato wa kumsajili straika huyo, ambaye anatarajiwa kutambulishwa na klabu hiyo hivi karibuni.
Akizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam, Ofisa Habari wa Yanga, Ali Kamwe, alithibitisha kuwa klabu yao inafanya usajili wa kuboresha kikosi chao katika kipindi hiki cha dirisha dogo.
Kulingana na ripoti ya IPP Media, Kamwe alisema, "Tumeanza na usajili wa Israel Mwenda kwa mkopo hadi mwisho wa msimu kutoka Singida Black Stars.
Hata hivyo, kuna wachezaji wengine ambao tutawongeza na mmoja wao atakuwa gumzo kubwa."
Kamwe alifafanua kuwa mchakato wa kumsajili Rupia ulikuwa mgumu, lakini sasa umefikia mwisho na wanategemea kumtangaza mchezaji huyo katika siku chache zijazo.
"Usajili huu hauna mbwembwe, lakini tutawashangaza wengi," aliongeza Kamwe.
Mashabiki wa Yanga sasa wanangojea kwa hamu kutaka kujua ni lini mchezaji huyo atatangazwa rasmi na klabu yao.