Edward Kinabo, aliyekuwa Mratibu wa Habari na Mawasiliano wa timu ya kampeni ya Freeman Mbowe katika uchaguzi wa Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Taifa, ameweka wazi maneno mazito ya Mbowe baada ya kushindwa na Tundu Lissu katika kinyang’anyiro hicho.
Kupitia andiko lake la karibuni, Kinabo amesema aliguswa sana na hekima, utulivu na ukomavu wa kisiasa uliooneshwa na kiongozi huyo muda mfupi baada ya matokeo yasiyo rasmi kujulikana.
Katika mazungumzo yaliyofanyika Januari 22, 2025, ndani ya chumba cha hadhi maalumu ‘VIP’ cha Mlimani City ambako kulikuwa kukifanyika Mkutano Mkuu wa CHADEMA, badala ya Mbowe kufarijiwa na wafuasi wake, ndiye aliyewapa moyo na kuwaeleza kuwa kushindwa kwake hakupaswi kuwakatisha tamaa wala kuwafanya waachane na chama.
"Msije mkawaza kuacha siasa au kuacha Chama hiki eti kwa sababu mimi mliyeniunga mkono nimeshindwa. Wala msitake kuususia au kujaribu kuukomoa uongozi huu uliochaguliwa kwa sababu tu mimi nimeshindwa. Hapana. Msifanye hivyo. Najua na ninyi mmekuwa na ndoto zenu za kisiasa kupitia chama hiki. Ni lazima maisha mengine yaendelee. Ni lazima muendelee na ndoto zenu. Endeleeni kushikamana na Chama. Endeleeni kupigania ndoto zenu katika siasa, na endelezeni ndoto ya Chama hiki ya kuwakomboa Watanzania,” alinukuliwa Mbowe akisema.
Kwa mujibu wa Kinabo, kauli hiyo ya Mbowe inathibitisha kuwa hakuwania nafasi ya uenyekiti kwa maslahi binafsi, bali kwa maslahi ya chama na taifa.
Aidha, Kinabo anasema maneno ya Mbowe ni tofauti na yale ambayo mara nyingi husemwa na wanasiasa wengi ambao hujionesha kuwa wastahimilivu hadharani lakini hubadilika faragha. Kwa Mbowe, alibaki na msimamo wake ndani na nje ya vikao, akihimiza mshikamano badala ya mpasuko.
"Viongozi na wanasiasa wengi huonesha busara na hekima ya kimaigizo hadharani, halafu huenda kunoa upanga sirini, lakini haikuwa hivyo kwa Mbowe. Bado alikuwa ni yule yule hata tulipoketi naye faragha nyuma ya pazia. Alimaanisha hadharani na alimaanisha sirini pia," anasema Kinabo.
Kwa mujibu wa Kinabo, hatua hiyo ya Mbowe inathibitisha ukomavu wa kisiasa, kwani alikubali matokeo na akawahimiza wafuasi wake waendelee kupambana kwa ajili ya CHADEMA.