Beyonce Ang'ara Tuzo za Grammy 2025

Beyonce Ang'ara Tuzo za Grammy 2025


Mwanamuziki mashuhuri Beyonce amepewa heshima kubwa katika tasnia ya muziki wa country baada ya kushinda tuzo ya Albamu Bora ya Muziki wa Country.


Tuzo hiyo ilikabidhiwa na mwanamuziki Taylor Swift katika kilele cha Tuzo za Grammy 2025 zilizofanyika Crypto.com Arena, Los Angeles, Marekani.


Beyonce, mwenye umri wa miaka 43, alishinda tuzo hiyo kwa albamu yake *Cowboy Carter*. Tuzo hiyo ilitolewa na Taylor Swift, mwenye umri wa miaka 35, ambaye pia ni mwimbaji wa kibao *Red*.


Katika kipengele hicho, Beyonce aliwashinda wasanii mashuhuri wakiwemo: Chris Stapleton - *Higher*, Kacey Musgraves - *Deeper Well*, Lainey Wilson - *Whirlwind*, na Post Malone - *F-1 Trillion*.


Beyonce awali alinyimwa tuzo hiyo na Chama cha Muziki wa Country (CMA) mnamo Septemba 2024, hivyo ushindi huu ulikuwa mshangao mkubwa kwake. Alionekana kutoamini baada ya Taylor kutangaza ushindi wake, huku akigeuka kuwaangalia binti yake, Blue Ivy, na mumewe, Jay-Z.


Katika hotuba yake ya kushukuru, Beyonce alisema: *"Ee Mungu wangu. Wow. Sikutegemea kabisa hili. Wow. Nataka kumshukuru Mungu. Ee Mungu wangu. Kwamba bado ninaweza kufanya kile ninachokipenda baada ya miaka mingi. Ee Mungu wangu. Ningependa kuwashukuru wasanii wote wa country walioukubali albamu hii. Tulifanya kazi kwa bidii sana."*


*Nadhani wakati mwingine, aina ya muziki ni kama neno baridi la kutufanya tusalie mahali fulani kama wasanii, lakini ningependa kuwahimiza watu wafanye kile wanachokipenda na wawe na uvumilivu. Wow.*


Alimalizia hotuba yake kwa kuwashukuru familia yake, akiwemo binti yake Blue Ivy, na kila mtu aliyeshiriki katika mradi huo uliopongezwa na wakosoaji wa muziki. Beyonce alisema: *"Ningependa kuwashukuru familia yangu nzuri. Wasanii wote waliokuwa washirika katika albamu hii. Asanteni. Albamu hii isingekuwepo bila ninyi. Ningependa kumshukuru Mungu tena, na mashabiki wangu. Bado nipo katika mshangao, kwa hivyo asanteni sana kwa heshima hii."*

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad