Dickson Job Awatega Mabosi Wake, Kitawaka Wakati Wowote




Nahodha msaidizi wa Yanga, Dickson Job amewatega mabosi wake kutokana na kuanza kuhesabu siku kabla ya mkataba alionao kumalizika.

Ofa kadhaa zimeanza kumiminika kwa mchezaji huyo jambo linalowapa kazi mabosi wa Yanga kukuna vichwa ili kumbakisha kutokana na umuhimu wa beki huyo anayeunda ukuta sambamba na Ibrahim Bacca na Bakari Mwamnyeto.

Ipo Hivi. Job amebakiza mechi 13 za ligi kwa mujibu wa mkataba alionao baada ya kuitumikia timu hiyo kwa misimu minne mfululizo.

Mchezaji huyo aliyejiunga na Yanga 2021 akitokea Mtibwa Sugar anamalizia msimu wa nne baada ya mitatu kucheza kwa mafanikio akitwaa mataji ya Ligi Kuu, Ngao ya Jamii na Kombe la Shirikisho na kuvaa medali ya Kombe la Shirikisho Afrika baada ya timu hiyo kucheza fainali.

Chanzo cha kuaminika kutoka kwa mtu wa karibu wa mchezaji huyo kimeliambia Mwanaspoti kuwa, tayari nahodha huyo msaidizi wa Yanga ameanza kupokea ofa kutoka nje ya nchi huku kipaumbele cha kwanza kikiwa ni kwa waajiri wake.

“Ni kweli mkataba wake unaisha mwisho wa msimu huu. Tayari ofa mbalimbali kutoka nje ya Tanzania zimeanza kumiminika. Kwa taarifa nilizozipata hadi sasa timu tatu zimeonyesha nia ya kumhitaji lakini muda haujakaa vizuri kwa ajili ya kuzungumza,’’ alisema mtu huyo.

“Kuhusiana na suala la kuitwa mezani na Yanga juu ya kuanza mazungumzo ya mkataba mpya hilo sina uhakika nalo, lakini ninachofahamu ofa tatu zimetua mezani kwa uongozi unaomsimamia mchezaji huyo.”

Wakati ofa hizo zikitajwa kuhusiana na kutaka kumng’oa beki huyo namba moja wa Yanga na timu ya taifa, inaelezwa kuwa mchezaji huyo kipaumbele chake ni kuipa nafasi Yanga kutokana na namna ilivyomuamini na kumpa nafasi ya kucheza tangu amejiunga nayo akitokea Mtibwa Sugar.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad