Mjasiriamali bilionea Elon Musk ameibua mvutano mpya na kiongozi wa chama cha Economic Freedom Fighters (EFF), Julius Malema, akipendekeza kwamba Malema atangazwe kuwa mhalifu wa kimataifa.
Mvutano huu umetokana na video ya Malema akidai kuwa chama cha Democratic Alliance (DA) kinawaunga mkono viongozi wake wa kizungu pekee, jambo ambalo Musk amepinga vikali.
Katika hotuba yake, Malema alisikika akisema:
"Hawa watu, ukitaka kuwagusa vilivyo, mpige mzungu. Wanaumia sana kwa sababu umemgusa mzungu. Si kwamba Mashaba na Solly hawataguswa, wataguswa, usijali. Lakini tunaanza na uzungu huu, tunakata koo la uzungu."
Musk amejibu kupitia mtandao wa kijamii X (zamani Twitter), akidai kuwa Malema anahamasisha mauaji ya Wazungu wa Afrika Kusini na hivyo anapaswa kupigwa marufuku kimataifa na kuwekwa chini ya vikwazo.
Malema, kwa upande wake, amesema hawezi kutishwa na wito wa Musk wa kumwekea vikwazo na kumtaja bilionea huyo kuwa "mtoto aliyebembelezwa sana".
Kiongozi huyo wa EFF amesisitiza kuwa ataendelea kutetea haki za watu weusi, hata kama hatua hiyo itawakasirisha viongozi wenye ushawishi katika jamii ya kimataifa.
Mvutano kati ya Musk na Malema si jambo jipya. Mwaka 2023, Musk alimshutumu Malema kwa kuimba wimbo wa "Kill the Boer" wakati wa sherehe ya kutimiza miaka 10 ya chama cha EFF, akidai kuwa ni uchochezi wa mauaji ya wakulima wa kizungu.