Zaidi ya watu 700 wameuawa na wengine 2,800 kujeruhiwa katika mapigano makali mjini Goma tangu Jumapili, huku waasi wa M23 wakidhibiti mji huo mkuu wa jimbo la Kivu Kaskazini. Ripoti za UN zinaonyesha kuwa waasi hao sasa wanasonga kuelekea Bukavu, mji mkuu wa Kivu Kusini, hali inayoongeza wasiwasi wa vita zaidi.
Serikali ya DRC inaituhumu Rwanda kwa kusaidia waasi hao kwa lengo la kuchochea mabadiliko ya utawala, madai ambayo Rwanda imekanusha. Jeshi la DRC limeweka ulinzi kati ya Goma na Bukavu kuzuia mashambulizi zaidi, huku raia wakijitolea kutetea mji wao.
Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) imeahidi kuendelea kuisaidia DRC kulinda uhuru wake, ikituma wanajeshi wa kulinda amani. Hata hivyo, wanajeshi 16 kutoka mataifa ya kusini mwa Afrika wameuawa katika mapambano na waasi wa M23.
Mgogoro huu unazidi kuzorotesha hali ya kibinadamu, huku wakazi wa Goma wakikabiliwa na uhaba wa chakula, maji safi, na dawa. UN inakadiria kuwa zaidi ya watu 400,000 wamekimbia makazi yao tangu mwanzo wa mwaka huu.