Imamu wa kwanza duniani aliyejitangaza hadharani kujihusisha na mapenzi ya jinsia moja, Muhsin Hendricks (57), ameuawa kwa kupigwa risasi nchini Afrika Kusini huku ripoti zikisema ameuawa baada ya kufungisha ndoa ya Watu wanaojihusisha na mapenzi ya jinsia moja.
Imamu huyo alikuwa anaongoza Msikiti mmoja JijiniCape Town uliolenga kuwa mahali salama na kimbilio kwa Waumini wa kiislamu wanaojihusisha na mapenzi ya jinsia moja na wale waliotengwa na jamii ambapo alipigwa risasi Jumamosi asubuhi baada ya gari alilokuwa akisafiria karibu na jiji la kusini la Gqeberha kushambuliwa.
Polisi wamesema “Washukiwa wawili wasiojulikana wakiwa wamefunika nyuso zao walitoka kwenye gari nyingine na kuanza kulimiminia risasi nyingi gari hilo”
Habari za kifo cha Hendricks zimeleta mshtuko mkubwa katika jamii ya Watu wanaojihusisha na mapenzi ya jinsia moja (LGBTQ+ ) na kwingineko, huku kukitolewa salamu nyingi za rambirambi kutoka sehemu mbalimbali za dunia.
Taarifa za tukio hilo zimeonekana kupitia video za CCTV zilizosambaa kwenye mitandao ya kijamii ambapo video hiyo inaonesha gari likisimama na kuziba njia ya gari alilokuwamo Hendricks kabla ya kuanza kushambuliwa.