Jude Okoye, kaka mkubwa na meneja wa zamani wa kundi la muziki lililovunjika, P-Square, amefikishwa mahakamani na Tume ya Kupambana na Uhalifu wa Kifedha (EFCC) kwa tuhuma za utakatishaji wa ₦1.38 bilioni, Tsh bil 2.2, na euro 34,537.59, zaidi ya milioni 92 za Kitaznania. Kesi hiyo ilisikilizwa mbele ya Jaji Alexander Owoeye katika Mahakama Kuu ya Shirikisho jijini Lagos, huku kampuni yake, Northside Music Ltd., pia ikikabiliwa na mashtaka saba.
Kesi hii inazidi kuongeza mvutano katika familia ya Okoye, ambayo imekuwa na migogoro ya muda mrefu. Ugomvi kati ya ndugu hao ulianza mwaka 2017 walipotengana, na ukazidi kuwa mkali mwaka 2024 baada ya Paul kudai kuwa Peter alimripoti yeye na Jude kwa EFCC kwa madai ya ubadhirifu wa fedha. Hata hivyo, Peter alikanusha tuhuma hizo, akisema hakuwahi kumripoti ndugu yake na kudai kuwa Jude ndiye mlengwa mkuu wa uchunguzi huo.
Ripoti za uchunguzi zinaonyesha kuwa Northside Music Ltd. imekuwa ikihamisha mirabaha ya P-Square kwenye akaunti ya siri kwa miaka kadhaa. Fedha hizo zilidaiwa kupitishwa kwenye maduka ya kubadilishia fedha kabla ya kuhamishiwa katika akaunti binafsi ya Jude. Kinachoshangaza ni kwamba mara baada ya fedha hizo kuingia kwenye akaunti ya Jude, ziligawanywa kwa usawa na Paul huku Peter akiachwa nje ya mgao huo.
Kwa sasa, kesi hiyo inasubiri tarehe ya kusikilizwa rasmi mwezi Aprili, huku wadau wa tasnia ya burudani wakifuatilia kwa karibu maendeleo yake.
Je, watu maarufu kwenye sekta ya burudani wanapaswa kuchunguzwa kwa ukali zaidi kuhusu masuala ya kifedha?Powered By: @solutionsarinsurancebrokerltd