Wakati Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) ikiapa kuurejesha Mji wa Goma, jiji lenye takriban watu milioni 3, kutoka mikononi mwa waasi wa M23, imeendelea kuishutumu Rwanda kwa madai ya kutuma wanajeshi huko kuwaunga mkono waasi hao.
Hata hivyo, katika mahojiano maalumu na CNN, Rais wa Rwanda, Paul Kagame, ambaye amekanusha mara kadhaa tuhuma hizo, alisema hajui kama wanajeshi wa nchi yake wako mashariki mwa Kongo ambako mapigano kati ya kundi la M23 na vikosi vya Kongo yanaendelea.
Kagame alisisitiza kuwa Rwanda itafanya kila linalowezekana kujilinda, huku akiishutumu Afrika Kusini kwa madai ya kutuma wanajeshi wake mashariki mwa DRC kwa lengo la kutafuta madini.
Katika hatua nyingine, Muungano wa waasi wa Alliance Fleuve Congo (AFC), unaojumuisha waasi wa M23, umetangaza kusitisha mapigano kuanzia leo Februari 4.
Taarifa inayodaiwa kuwa ya kundi hilo, iliyosambaa kwenye mtandao wa X (Twitter), ilieleza kuwa usitishaji huo wa mapigano umefanyika kwa sababu za kibinadamu.
Katika taarifa hiyo, waasi hao wameilaumu serikali ya Kinshasa kwa kusababisha athari kubwa za kibinadamu kutokana na uvamizi wake.
Waasi wa M23, ambao hivi karibuni walizidisha mashambulizi yao mashariki mwa Kongo na kudhibiti Mji wa Goma, mji mkuu wa Jimbo la Kivu Kaskazini, wiki iliyopita, wameendelea kusababisha taharuki kubwa.
Mapigano makali kati ya vikosi vya serikali na waasi hao yamesababisha vifo na majeruhi wengi.
Kwa mujibu wa Wizara ya Afya ya Kongo, kufikia Januari 30, maiti 773 zilikuwa zimehifadhiwa kwenye vyumba vya kuhifadhia maiti huko Goma, huku zingine zikisalia mitaani kutokana na msongamano mkubwa.
Muungano wa waasi umelaani vikosi vya jeshi la Kongo kwa kutumia ndege za kijeshi katika uwanja wa ndege wa Kavumba, wakidai kuwa zinaangusha mabomu yanayoua raia katika maeneo waliyoyadhibiti.
Hata hivyo, waasi hao wamesisitiza kuwa hawana nia ya kuteka Bukavu, mji mkuu wa Jimbo la Kivu Kusini, au maeneo mengine.
"Tunasisitiza dhamira yetu ya kulinda na kutetea raia pamoja na maeneo yetu yaliyoko chini ya udhibiti wetu," ilisema taarifa yao.