Kanye West (Ye) ameibua tena mjadala mkali mtandaoni baada ya kuposti ujumbe mrefu kwenye X (zamani Twitter) Jumanne hii, akizungumzia madai yake ya kutengwa na baadhi ya watu wenye ushawishi wa Kiyahudi.
Katika mfululizo wa jumbe zake, Kanye alikumbusha tukio la miaka miwili iliyopita aliposema “Deathcon 3 on the Jews,” kauli iliyosababisha kufungiwa kwenye mitandao ya kijamii na kupoteza mikataba mikubwa ya kibiashara.
Hata hivyo, sasa anadai kuwa licha ya kusukuma kila “wazo linaloweza kufutwa,” hakuna aliyemzuia, kumtisha, au kumlazimisha kubadili msimamo wake.
“Nilisema mambo haya yote yasiyo sahihi kisiasa, na hakuna aliyeniangamiza. Na siku iliyofuata, nilitengeneza dola milioni 40 kutoka kwenye biashara zangu tofauti,” aliandika.
Kanye pia alieleza kuwa alimpoteza mbunifu wake wa Yeezy, Simon, na stylist wake Malcolm, kwa sababu ya msimamo wake. Lakini anasema ana matumaini kuwa siku moja wataelewa kwa nini alifanya aliyoyafanya.
Katika ujumbe wake, Kanye alizungumzia pia kuhusu tovuti ya kampuni yake ya Yeezy kuondolewa kutoka Shopify, lakini badala ya kuiona kama hasara, aliitaja kama ushindi.
“Niliwachukia Shopify kila wakati. Nilijua wangefanya jambo la kipumbavu kama hili. Wana udhibiti wa soko lako na wanakusanya data zako zote, jambo linalowafanya kuwa na thamani kubwa huku wakikupora wewe,” aliandika, akimtaja mkurugenzi wa Shopify, Harley Finkelstein.
Pia alizungumzia wazo lake la fulana yenye alama ya swastika, akisema kuwa alivutiwa na jinsi ishara hiyo imekuwa na maana tofauti katika tamaduni mbalimbali, licha ya kuhusishwa sana na Ujerumani ya Nazi.
Kwenye ujumbe wake huo pia Kanye amethibitisha kushiriki kwenye album jayo ya The Game.