SIMBA inashuka uwanjani ugenini Jumatano hii dhidi ya Namungo kwenye mchezo mgumu wa Ligi Kuu Bara lakini Kocha wa Wekundu hao, Fadlu Davids kuna ishu kaishitukia kuhusu watani wao wa jadi, Yanga. Fadlu ambaye amekuwa na mbinu kali kwenye mechi zake amesema kuna haja ya kufanya mabadiliko makubwa kwenye kikosi ili kuhakikisha kinafunga mabao mengi kwa kuwa wapinzani wao wameshawaacha nyuma kwa idadi kubwa ya mabao na hilo linaweza kuwanyima ubingwa endapo watalingana pointi mwishoni.
.
“Ili tusikose ubingwa kwa namna yoyote ile, lazima idadi ya mabao iongezeke kwenye mechi zetu, katika msimamo wa Ligi Kuu hasa nafasi ya kwanza ambayo wapo wapinzani wetu (Yanga), kumekuwa na mabadiliko makubwa kwao, kila mechi zikichezwa.
.
“Kuna mabadiliko ninayoyafanyia kazi haraka sana baada ya kuona wapinzani wetu, mechi zinazokuja ikiwemo hii dhidi ya Namungo naamini zitakuwa na matunda, tunakwenda mwisho wa msimu kila timu inapambania malengo yake nasi lazima tuhakikishe tunabadilisha baadhi ya vitu,”
.
“Ukiona mbio za ubingwa bádo zipo wazi sana, lolote linaweza kutokea, tunaendelea kushinda mechi zetu hatutaki kurudia makosa ya kuangusha pointi kirahisi, lakini lazima tufunge mabao ya kutosha kwa kuwa huko mbele yanaweza kuwa sehemu ya timu kutwaa ubingwa msimu huu,” alisema
.
Ikumbukwe Simba ilikosa ubingwa kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa msimu wa 2016/2017, ambapo Yanga iliiubeba baada ya timu zote mbili kukusanya pointi 68, lakini Yanga ilichukua ubingwa huo baada ya kufunga mabao 57 na kuruhusu 14. huku Simba ikifunga 50 na kuruhusu 17 tu.