Dar es Salaam. Meneja wa Hamisa Mobetto, Doctar Ulimwengu amesema suala la ndoa ya Hamisa na Aziz Ki ni ukweli mtupu na siyo kiki kama baadhi ya watu wanavyodhani.
Akizungumza na Mwananchi leo Februari 10, 2025, Ulimwengu amesema wawili hao wanapendana na sasa wameona ni muda wa kuishi pamoja.
Doctar Ulimwengu akiwa na Hamisa Mobetto
"Siyo kiki ni ndoa kabisa, wale ni wapenzi Mungu amewabariki sasa wanaoana. Ndoa Februari 16, 2025, sherehe tarehe 19.
"Hamisa anajua kipi kimefanya yeye na Aziz wakapendana, watu wanaweza wakaona uzuri wa Hamisa lakini kumbe Aziz kaangalia akili. Mimi ninachojua wamependana na wameridhiana na wameona wanafaa kuishi pamoja,"amesema.
Amesema anamtakia Hamisa maisha mema yenye baraka katika ndoa anayotarajia kuingia hivi karibuni.
"Mungu awajalie furaha amani, upendo na mafanikio sababu wote wana majina makubwa na biashara kubwa ndoa yao iwe ya baraka wasiruhusu shetani aweze kuingia,"amesema.
Mbali na hayo katika chapisho linalosambaa kwenye mitandao ya kijamii linaeleza kuwa Februari 15,2025 itakuwa siku ya kupokea mahari, Februari 16 Nikkah (ndoa) na Februari 19 ndiyo itafanyika sherehe ya wawili hao.
Ulimwengu anasimamia chapa za mastaa kama Hamisa Mobetto, Jux, Idris Sultan, na hapo awali alimsimamia Jay Mondy na wengineo.