Jeshi la Polisi mkoa wa Mtwara linawashikilia watuhumiwa wawili ambao ni Mwalimu wa Shule ya Msingi Nanyani iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara mkoani Mtwara, Mohamed Ally Kajao (34) na Dickson Paul Tamba (27), mjasiriamali, mkazi wa Mkuti Chini Machinjioni wilayani Masasi, kwa kujihusisha na mapenzi ya jinsi moja.
Akitoa taarifa hiyo kwa waandishi wa habari Februari 12, 2025 Kamanda wa Polisi mkoa wa Mtwara Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi Issa Suleiman, amesema tukio hilo lilifanyika Januari 2025 katika nyumba ya kulala wageni (jina limehifadhiwa) ambapo Dickson Tamba aliruhusu kuingiliwa na Mohamed Ally Kajao, kisha kunakili picha mjongeo (video) na kuzisambaza kwenye mitandao ya kijamii.
Pia Jeshi hilo linamshikilia mlinzi wa Kampuni ya Kiwango Security, mkazi wa Magomeni wilaya ya Mtwara kwa tuhuma za kumlawiti mtoto wa kike (10) ambaye ni mwanafunzi wa darasa la nne mkazi wa Magomeni. Pia linamshikilia na Mkulima Ahmad Mohamed (39) mkazi wa Libobe wilaya ya Mtwara kwa tuhuma za kumbaka mtoto wa kike (04) mkazi wa Libobe.
Ameongeza kuwa kwa kipindi cha kuanzia Januari 1, 2025 hadi Januari 31,2025 kupitia doria, misako na operesheni iliyofanyika kwa kipindi hicho Jeshi la Polisi mkoani humo lilifanikiwa kuwakamata watuhumiwa 23 kwa tuhuma za kujihusisha na kubaka, kupatikana na pombe haramu ya moshi (gongo), wizi, kuchoma nyumba moto, kupatikana na nyara za serikali pamoja na kupatikana na dawa zidhaniwazo kuwa ni za kulevya aina ya bangi.