Polisi Mbeya Wakamata Mtandao wa Uuzaji Bangi...




Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya limefanikiwa kuvunjilia mtandao wa usafirishaji na biashara ya dawa za kulevya, baada ya kuwakamata watuhumiwa Innocent Mendrad Komba (48) na Zawadi Jackson Mwakijolo (32) wakiwa na kilogramu 142 za bhangi.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, SACP Benjamin Kuzaga, watuhumiwa hao walikuwa wakisafirisha dawa hizo kutoka Kasumulu, Kyela, wakizificha kwenye mifuko ya sandarusi iliyojaa nguo za mtumba ndani ya gari aina ya Toyota Vista lenye namba T.969 BLZ. Polisi walifanikiwa kuwakamata watuhumiwa hao kabla ya kufanikisha biashara hiyo haramu.

Katika operesheni hiyo, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya pia limewakamata jumla ya watuhumiwa 979 kwa makosa mbalimbali ndani ya mwezi Januari pekee, ikiwemo watuhumiwa wa ujangili, akiwemo Dadrahimu Aladad (74), Daud Masengwa (55), Mkombe Mathias (34) na Dotto Daimon (39) waliokutwa na jino moja zima na vipande viwili vya meno ya tembo, wakitafuta mteja.

Wengine waliokamatwa ni wale waliokutwa na silaha kinyume cha sheria, wakiwemo Faraja Majengo (19), Fidelis Mdutu (25) na Charles Mfilinge (39) waliokamatwa na bunduki mbili aina ya Gobole, goroli 228, fataki 14, vipande vya nondo 16 na unga wa baruti makopo mawili.

Kamanda Kuzaga amesisitiza kuwa Jeshi la Polisi litaendelea na misako na doria ili kuhakikisha wananchi wanakuwa salama, huku akitoa wito kwa jamii kushirikiana na vyombo vya ulinzi kwa kutoa taarifa za kihalifu kwa wakati.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad