Wasanii wengi wa Tanzania wanakumbana na changamoto kubwa katika kutekeleza maonyesho yao (live performances), na moja ya sababu kuu ni tabia ya kuongeza vipengele ambavyo havipo kwenye wimbo. Hii mara nyingi huathiri ubora wa perfomance zao na kuwafanya waonekane kama hawajajiandaa vya kutosha.
Moja ya makosa yanayofanyika ni kubadilisha melodi au flow ya wimbo kwa namna isiyopangiliwa, jambo linaloweza kuwachanganya mashabiki wanaotegemea kusikia kile walichozoea kwenye wimbo. Wakati mwingine, wasanii hujaribu kuongeza maneno, sauti za ziada, au miondoko isiyoendana na mpangilio wa awali wa wimbo, hali inayoweza kufanya uwasilishaji wao usiwe na mvuto kama ulivyotarajiwa.
Pia, baadhi ya wasanii hushindwa kudhibiti matumizi ya “playback” au “live band” kwa ufanisi, jambo linalopelekea maonyesho yao kuonekana yasiyo na uthabiti. Badala ya kuzingatia uimbaji wa moja kwa moja kwa usahihi, wengine hujaribu kufunika mapungufu yao kwa kelele au kupiga kelele zisizo na mpangilio, hali inayopunguza ubora wa maonyesho yao.
Kwa upande wa mashabiki, wanapoenda kwenye show, wanatarajia kuona na kusikia kile walichokipenda kwenye wimbo. Hivyo, wasanii wanapaswa kuelewa kuwa kubadilisha sana uwasilishaji wa nyimbo zao kunaweza kupunguza mvuto wa perfomance zao.
NYIMBO ZETU NI NZURI SANA ILA TUNAZIIMBA VIBAYA STEJINI.