Timu ya msanii Jux imeomba ufafanuzi kutoka kwa waandaaji wa #TraceAwards baada ya posti yao iliyomtangaza Jux kama mshindi wa 'Tuzo ya Msanii Bora wa Tanzania' kuondolewa ghafla bila maelezo yoyote.
Kupitia ujumbe ulioandikwa na Docta Ulimwengu, timu ya Jux imesema kuwa kitendo hicho kimeleta mkanganyiko miongoni mwa mashabiki na washirika wa biashara wa msanii huyo, jambo ambalo linaweza kuathiri taswira yake kwenye sekta ya muziki.
"Tunachukulia jina na heshima ya Jux kwa umakini mkubwa. Kuondolewa kwa chapisho bila mawasiliano kumesababisha sintofahamu, na tunahitaji maelezo rasmi kuhusu suala hili," ujumbe huo ulieleza.
Timu ya Jux imeitaka Trace Awards kutoa maelezo ya wazi kuhusu sababu ya kuondolewa kwa tangazo hilo na hatua zinazochukuliwa kulitatua jambo hilo. Wameeleza kuwa uwazi katika masuala kama haya ni muhimu kwa wasanii na tasnia ya burudani kwa ujumla.