Jeshi la Polisi Mkoa wa Mtwara kwa kushirikiana na Vyombo vingine vya Dola pamoja na Benki kuu ya Tanzania tawi la Mtwara limewakamata Watuhumiwa watatu ambao ni Athuman Ramadhan Chitivi (35) Mwalimu wa Shule ya msingi Makome na Meneja wa Kampuni ya LBL Mtwara, Zacharia Emmanuel Zacharia (30) Mwalimu wa Shule ya sekondari Mbawala ambaye ni Meneja Msaidizi wa LBL na Mustapha Mussa Mweta (26), Mjasiriamali na Mwanachama wa kampuni hiyo.
Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Mtwara amesema Polisi ilipata taarifa za uwepo wa Kampuni iitwayo Leo Burnet London LBL MTWARA MEDIA CAMPANY LIMITED mbayo inayojihusisha na biashara ya kukusanya hela, kufanya malipo, kupata faida kubwa mitandaoni bila ya kuwa na leseni”
“Watuhumiwa hao wamekuwa wakijihusisha na biashara ya malipo kwa njia ya mtandao bila ya kuwa na leseni, kwa kutengezeza makundi ya WhatsApp kwa ajili ya kuwaunga Wanachama ambao wamekwishalipia na kueleza kuwa wamekuwa wakituma link maalumu kwa Wateja ili kujiunga mtandaoni na kisha Wateja kutakiwa kulipa fedha kati ya Tsh. 50,000 na Tsh. 540,000, baada ya kulipa wanatakiwa kuangalia matangazo ya filamu kupitia simu zao na wakishaangalia matangazo wanapata pesa kila Wanachama kulingana na kiasi walichojiunga nacho”
“Watuhumiwa hao wamekuwa wakifanya biashara hiyo bila ya kuwa na kibali kutoka Benki kuu ambayo ndio yenye mamlaka ya kuruhusu biashara ya aina hiyo, aidha biashara hii haitambuliki na Benki kuu ya Tanzania na kwamba vipo viashiria vya utapeli, napenda kutoa rai kwa Wananchi wa Mkoa wa Mtwara kuacha kujihusisha na biashara za fedha za mitandao ambazo sio rasmi, hazitambuliki na hazina leseni kutoka BoT kwa kuwa ni kosa kisheria na kujihusisha na biashara bila ya kuwa na leseni na kuna uwezekano mkubwa wa kuibiwa fedha zao”