UONGOZI wa Yanga umeweka wazi sababu ya kiungo wao, Clatous Chama kukosa namba katika kikosi cha kwanza licha ya makocha watatu kupita katika kikosi hicho ambacho kwa sasasa kinaongozwa na Kocha Hamdi Miloud.
Tangu amejiunga na Yanga kwa msimu huu kiungo uyo hajaaminiwa kuanza kikosi cha kwanza tofauti na alivyokuwa simba hali ambayo inazua sintofahamu kwa mashabiki huku mchezaji huyo akidaiwa kutokuwa na furaha ndani ya timu hiyo.
Chama alisajiliwa na Yanga kwa mkataba wa mwaka mmoja kutokana na ubora aliouonesha alipokuwa Simba.
Ofisa Habari wa Yanga, Ali Kamwe amesema Chama ni miongoni mwa wachezaji bora na wakubwa, atapata nafasi ya kucheza kulingana na mahitaji ya kocha kutokana na kiwango chake hakuna timu ambayo haitamani kuwa na mchezaji kama huyo.
"Yanga tunajivunia kuwa na mchezaji wa aina ya Chama kwenye kikosi, kinachotokea kukosa nafasi tunapokwenda kwenye mechi husika mwalimu anakuwa na mipango mingine tofauti na yeye.
“Sio kwamba hana ubora na mchango kwenye klabu yetu, mchango wake ni mkubwa ila mipango ya mwalimu inahitaji wachezaji wa aina gani kulingana na timu pinzani,” amesema Ally kamwe.
Kamwe amesema Chama atapata nafasi ya kucheza kwa sababu wanakabiliwa na michezo mingi, ikiwemo Ligi Kuu Tanzania Bara na michuano ya Kombe la Shirikisho FA, ambayo anaamini Chama atapata nafasi ya kuonesha uwezo wake na kuisaidia timu kufikia malengo yake.