MABAO mawili aliyoyafunga kiungo nyota mshambuliaji wa Simba, Jean Charles Ahoua, juzi katika ushindi wa 6-0 dhidi ya Dodoma Jiji, unamfanya kunyatia rekodi mbili kwenye michezo minane iliyobaki ya Ligi Kuu Bara.
Nyota huyo aliyejiunga na Simba Julai 3, 2024 akitokea Stella Club d’Adjame ya kwao Ivory Coast, amebakisha bao moja tu na asisti nne, ili kuivunja rekodi yake ya msimu uliopita iliyomfanya kuibuka kidedea wa mchezaji bora (MVP) Ligi Kuu ya Ivory Coast.
Msimu huu pekee tayari nyota huyo amefunga mabao 12 akiwa ndiye kinara na kuchangia sita Assist’, huku msimu uliopita wakati akiwa na kikosi cha Stella Club d’Adjame alifunga mabao 12 na kusaidia upatikanaji wa mengine tisa.
Msimu huu Jean Ahoua amechangia mabao 18 ya Ligi Kuu ndani ya kikosi cha Simba kati ya 52 yaliyofungwa na timu nzima ambayo kwa sasa inashika nafasi ya pili kwenye msimamo na pointi 57, nyuma ya wapinzani wao Yanga wenye 58.
Nyota huyo aliyezitumikia timu za LYS Sassandra na Sewe Sports kisha kutua Stella zote za kwao Ivory Coast, ana uwezo wa kufunga na kutengeneza mabao, huku akicheza nyuma ya mshambuliaji na wakati mwingine akitokea winga ya kulia au kushoto.
Tangu atue kikosi cha Msimbazi, tayari ameivunja rekodi ya mabao ya Clatous Chama aliyoiweka msimu wa kwanza wa 2018-2019, akitokea Lusaka Dynamos FC ya kwao Zambia, alipofunga mabao saba na kuchangia mengine tisa katika ligi.
Kwa maana hiyo Ahoua amebakisha asisti tatu tu kuifikia rekodi ya Chama ya msimu wake wa kwanza japo ikiwa atafikisha nne ataivuka, ingawa anatakiwa kuende lea kuonyesha kiwango bora kama alivyofanya Mwamba wa Lusaka.