Baada ya kushindwa kupeleka timu uwanjani kwenye Derby ya Jiji la Cairo dhidi ya mahasimu wao Zamalek, klabu ya Al Ahly imetangaza kurudisha viingilio vya mashabiki waliokuwa wamenunua tiketi kwa ajili ya kushuhudia mtanange huo.
Taarifa ya Ahly imeeleza kuwa klabu hiyo inafanya mchakato wa kuwasiliana na kampuni inayohusika na ununuzi wa tiketi ndani ya saa chache zijazo ili kuweka utaratibu wa kurejesha fedha hizo kwa Mashabiki wote waliokuwa tayari wamenunua tiketi kwa ajili ya mchezo huo.
Awali Mabingwa hao wa kihistoria wa klabu Bingwa Afrika waligomea mchezo huo wakiishinikiza Shirikisho la soka Nchini Misri EFA kuteua waamuzi wa kigeni kuchezesha mchezo huo wakigomea Derby hiyo kubwa barani Afrika kusimamiwa na Waamuzi wa ndani.
Zamalek imechukua ushindi wa mezani wa mabao 3-0 pamoja na pointi tatu ambapo uamuzi huu umefuata kanuni za ligi ambazo zinatoa ushindi kwa timu iliyofika uwanjani ikiwa mpinzani wake hajajitokeza bila sababu inayokubalika.