JESHI la Polisi Mkoa wa Tanga limetoa sababu ya kuendelea kumshikilia bondia maarufu nchini Hassan Mwakinyo (29), anayetuhumiwa kumshambulia mkazi wa jijini Tanga Mussa Ally akimtuhumu kuwa ni mwizi.
Akizungumza na waandishi wa habari Ofisini kwake leo Jumatatu Machi 10, 2025, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Almachius Mchunguzi amesema Mwakinyo anatuhumiwa kumshambulia na kumjeruhi Mussa Ally ambae anadai ni mvuvi alipopita kwenye makazi yake huku akibainisha kuwa uchunguzi utakapokamilika atatoa taarifa kwa vyombo vya habari ikiwa ni sambamba na kumfikisha mahakamani ili ajibu tuhuma zitakazomkabili.
Kamanda Mchunguzi amesemna wamemkamata Mwakinyo kwa tuhuma za kumjeruhi mvuvi, ambapo ni tuhuma za jinai huku akifafanua kuwa mtu yeyote akifanya makosa kama hayo bila kuangalia nafasi yake kwenye jamii, anatakiwa kuchukuliwa hatua za kisheria na suala la umaarufu haliwezi kubadili kile kilichotendeka.
“Jeshi la polisi Mkoa wa Tanga linamshikilia Hassan Mwakinyo (29) mkazi wa Sahare jijini Tanga kwa kumshambulia na kumjeruhi Mussa Ally mkazi wa eneo hilo ambae ni mvuvi, uchunguzi wa tukio hili unaendelea na ukikamilika mtuhumiwa atapelekwa mahakamani,”—amesema Mchunguzi.