Mara baada ya Mkaguzi na Mdhibiti wa hesabu za Serikali nchini (CAG) Dkt. Charles Kichere, juzi kuwasilisha ripoti ya fedha kwa mwaka 2023/2024 mbele ya Rais Samia na kuonekana kuna deni la trilioni 97.35, CCM wameamua kuvunja ukimya kwa kutoa maoni juu ya deni hilo.
Makamu mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Steven Wasira ameeleza kuwa nchi inakopa kwa ajili ya kufanya mambo ambayo Tanzania itaishia nayo. Na faida zake zitakuwepo kwa miaka mingi kwa kizazi cha sasa na hata kijacho, huku akisisitiza kuwa deni lililopo la Tsh. trilioni 97 sio kwamba lote limekopwa na Rais wa sasa Samia Suluhu Hassan, bali limekuwepo tangu enzi za Rais wa kwanza Hayati Mwalimu Julius Nyerere.
Wasira ametoa kauli hiyo alipokuwa akiongea na wanachama pamoja na viongozi wa CCM Wilaya ya Maswa mkoani Simiyu, katika kikao cha ndani ikiwa ni sehemu yake ya kikazi mkoani humo yenye lengo la kukagua uhai wa chama, utekelezaji, wa ilani ya uchaguzi ya CCM na kusikiliza kero za wananchi.
Wasirra ameeleza kuwa tunakopa ili kufanya jambo ambalo tutaishi nalo na faida zake kwa miaka mingi kwa kizazi hiki na hata kizazi kijacho. Ameongeza kuwa hilo deni sio kwamba amekopa Rais Samia trilioni 97, deni linaongezaka na madeni mengine ya zamani ambayo tulishakopa tangu enzi za Nyerere.
Utakumbuka mbali na madeni hayo, katika ripoti ya CAG, ilieleza baadhi ya sekta kudaiwa mabilioni ya pesa ikiwemo sekta ya umeme nchini TANESCO. Ambapo inadaiwa na kampuni ya IPTL bilioni 238. Mbali na hayo CAG alieleza katika matumizi ya fedha ya mwaka 2023/2024 kulikuwa kuna matumizi yasiyo ya lazima ya bilioni 371. Rais Samia alidai kuwa watafanyia kazi ripoti ya CAG.
Chanzo; Millard Ayo.