Aliyekuwa msemaji wa klabu ya Yanga, Haji Manara amezungumzia sakata la mechi ya dabi ya Kariakoo pamoja na kauli ya Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Wallace Karia, kuhusu ombi la Yanga SC la kutaka Bodi ya Ligi ijiuzulu.
Akizungumza na waandishi wa Habari, Manara ametoa wito kwa Kamati ya utendaji ya klabu hiyo kuitisha mkutano wa dharura kujadili kile kilichonukuliwa na Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) ndugu Wallece Karia juu ya watu wenye nia ovu ya kutaka kuharibu mpira wa Tanzania.
“Usitumie kiburi cha uongozi kuwadhalilisha wenzio kwasababu wametumia kanuni, bila heshima Karia unaukosea Mpira na unaikosea Yanga. Na viongozi wa Yanga najua hawawezi kukwambia kwasababu utawafungia na katika hili omba radhi kwa kufuta kauli zako za jana”——amesema Manara kufuatia kauli ya Rais wa TFF Wallace Karia
“Nazungumza kwaniaba ya wana Yanga tena ni mjumbe wa mktano mkuu kikanuni, kamati ya utendaji chini ya Rais wetu Hersi iitishe mkutano mkuu wa Dharura ajenda iwe moja tu kujadili hili sakata tutoe maazimio ya mkutano mkuu””——amesema Manara
Kauli ya Rais Karia iliyozua sintofahamu hiyo: “Taratibu tuziache zifuatwe, Lakini huwezi kusema bodi ijiuzulu. Hata wanaosema wawaambie na viongozi wao, hawastahili kujiuzulu? Vitu vingine vinafanyika kitoto, Kama watu wamechoka kucheza mpira basi wakaendelee na Sinema zao.”