Web

Hatua Zimechukuliwa Dhidi ya Makalla Kauli ya Chadema Kununua Virusi vya Ebola - Msajili Vyama

Hatua Zimechukuliwa Dhidi ya Makalla Kauli ya Chadema Kununua Virusi vya Ebola - Msajili Vyama


Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa imetoa majibu kwa chama cha ACT Wazalendo kuhusu ombi lao la kuchukuliwa hatua dhidi ya Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Amos Makalla.


Katika barua yake, Msajili ameeleza kuwa tayari ofisi yake ilishachukua hatua zinazostahili kwa mujibu wa Sheria ya Vyama vya Siasa, Sura ya 258, hata kabla ya kupokea ombi la ACT Wazalendo.


Akizungumza kupitia barua ya tarehe 25 Machi 2025 ambayo Jambo TV tumepata kuiona, Msajili wa Vyama vya Siasa, kupitia kwa Naibu wake Sisty Nyahoza, ameeleza kuwa ofisi yake hufanya kazi kwa mujibu wa sheria na kuchukua hatua zinazohitajika bila kusubiri mapendekezo kutoka kwa taasisi au mtu yeyote.


"Msajili anakushukuru kwa mapendekezo yako na anapenda ufahamu kuwa, Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa huchukua hatua katika matukio kama hayo kwa mujibu wa sheria, hata bila ya mapendekezo ya mtu au taasisi yoyote," imeeleza sehemu ya barua hiyo.


ACT Wazalendo, kupitia Katibu Mkuu wake, Ado Shaibu, walikuwa wamewasilisha barua kwa Msajili wa Vyama vya Siasa wakipendekeza hatua zichukuliwe dhidi ya Amos Makalla kutokana na kauli alizotoa kwenye mkutano wa hadhara mkoani Simiyu tarehe 22 Machi 2025 za madai kuwa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kinaendesha harambee ya kununua virusi vya M-pox na Ebola kwa lengo la kuzuia uchaguzi mkuu wa mwaka 2025. ACT ilizitaja kauli hizo kuwa za kizembe na zenye lengo la kuzua taharuki.


Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa haikufafanua hatua mahsusi ilizochukua dhidi ya malalamiko hayo lakini imeeleza kuwa inatekeleza wajibu wake kwa mujibu wa sheria.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad