Viongozi wa matawi ya @yangasc na Wazee wa klabu hiyo mkoani Dodoma wametoa tamko kali wakimtaka Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), @tanfootball Wallace Karia, kuomba radhi hadharani kwa kauli alizozitoa kufuatia kuahirishwa kwa mechi ya watani wa jadi, Simba na Yanga.
Wakizungumza na wanahabari Jijini Dodoma leo Machi 18, 2025 viongozi na wazee hao wameeleza kutoridhishwa kwao na maamuzi yaliyofanywa, wakidai kuwa wamepoteza imani na Karia na uongozi wake.
Mzee Abdalah Mtosa Ally kutoka Tawi la Chang’ombe amesema hakuna sababu ya kurudia mechi hiyo kwani tarehe 8 ilikuwa sahihi kwa mchezo huo kufanyika.
"Mimi kama mzee wa Yanga Dodoma, kwa masikitiko makubwa, hatuna imani na Karia kwani tunajua wazi hana mapenzi ya dhati na Yanga. Niwaombe viongozi wa juu kutoruhusu mechi hiyo kufanyika tena. Kama ni faini tuko tayari kulipa, lakini siyo kurudia mechi na Simba," amesema Bernard Mtengwa, mmoja wa wazee wa Yanga.
Naye Bodar Awadhi Ahmed, mzee mwingine wa Yanga, amesema kuwa uamuzi wa kuahirisha mechi hiyo umeleta mkanganyiko na sintofahamu kwa mashabiki wa soka, huku wengi wao wakipinga kufanyika upya kwa mchezo huo.
Aidha, viongozi hao wamesisitiza kuwa hawana tena imani na Karia kutokana na kauli zake walizodai kuwa zimewadhalilisha Wanayanga.
"Sisi msimamo wetu ni kutokurudia mechi. Kwanza Rais wa TFF ametudhalilisha Wanayanga, na kama ameshindwa mpira, arudi kwenye taaluma yake, kwani tunaijua," wamesema kwa msisitizo.
Kwa upande wake, Mratibu wa Yanga Dodoma, Elisha Ngwando, amemtaka Karia kuwaomba radhi Wanachama wa Yanga na wanamichezo kwa ujumla kwa maamuzi aliyofanya na kauli alizozitoa.
"Watu wametumia gharama kubwa, wengine wamelipia matangazo kwa ajili ya mechi hiyo," amesema Ngwando.
WanaYanga hao wameendelea kusisitiza kuwa hawataki mechi hiyo irudiwe, huku wakitoa wito kwa viongozi wa juu wa mpira nchini kuhakikisha haki inatendeka kwa klabu yao.