Web

House Girl Akamatwa Stand Akitorosha Kichanga cha Miezi Mitatu

Top Post Ad



Jeshi la Polisi mkoani Tabora linamshikilia Christina Nashoni (15), mfanyakazi wa ndani kutoka Kijiji cha Malagarasi, Kigoma, kwa tuhuma za kujaribu kutorosha mtoto mchanga wa miezi mitatu wa mwajiri wake, Beatrice Kiboma, mkazi wa Cheyo 'B' katika Manispaa ya Tabora.

Kwa mujibu wa wazazi wa mtoto huyo, Beatrice Kiboma na Dotto Mwalembe, binti huyo alifika nyumbani kwao Machi 18 kwa ajili ya kazi za ndani, lakini siku moja tu baadaye, Machi 19, alijaribu kutoroka na mtoto wao.

"Mchana wa tukio, binti huyo aliniaga kuwa anakwenda kuanika nguo nje huku akimbembeleza mtoto. Nilimwambia amlete mtoto ndani, lakini akasema atarudi naye baada ya kuanika nguo. Dakika chache baadaye, sikusikia tena sauti ya mwanangu, hivyo nikatoka nje na kwenda kwa majirani kutoa taarifa," alisema Beatrice Kiboma.

Mume wake, Dotto Mwalembe, alieleza kuwa alipokea simu kutoka kwa mke wake akiwa kazini, akilia na kueleza kuwa mfanyakazi wao mpya ametoweka na mtoto wao. "Nilitaka kwenda Polisi, lakini majirani walikwisha sambaza taarifa kwa madereva bodaboda na vituo vya mabasi. Bahati nzuri, wananchi walifanikiwa kumkamata kabla hajatoweka," aliongeza.

Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Tabora, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Richard Abwao, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa uchunguzi wa awali umebaini kuwa binti huyo alikusudia kurudi Kigoma na mtoto huyo.

"Tuna taarifa kuwa alipokuwa anaondoka kijijini kwao alidanganya kuwa ni mjamzito. Alipoanza kazi, alihisi kuwa kazi ni nyingi, hivyo akaamua kutoroka na mtoto kwa kisingizio cha kwenda kuanika nguo," alisema Kamanda Abwao.

Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi ili kubaini nia kamili ya msichana huyo na kuchukua hatua za kisheria.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.