Moses Phiri anasema alikuwa na wakati mzuri Simba hasa msimu wake wa kwanza wa 2022/23 aliomaliza akiwa na mabao 10 na alionyesha kiwango cha juu katika mashindano mbalimbali klabuni hapo.
"Isingekuwa kuumia ningemaliza na zaidi ya mabao 10, huenda ningeingia kuwania kiatu cha ufungaji na Fiston Mayele na Saido Ntibazonkiza ambao walimaliza na mabao 17. Niliufurahia ushindani ulivyokuwa mkubwa," anasema Phiri.
Anasema hakukaa muda mrefu Msimbazi kutokana na sababu za majeraha, akidai: "Ilifika wakati wa kuondoka na lilikuwa jambo zuri kwa kazi yangu, kwani mzunguko wa pili ambao sikuumalizia nilifunga mabao matatu, nilipitia majeraha ya hapa na pale na ni changamoto za kawaida katika kazi yetu."
Phiri anasema anakumbuka Simba ilimpa nafasi ya kuonyesha kipaji na kumkutanisha na watu wapya kama wachezaji, mashabiki, viongozi na makocha.
"Simba ni miongoni mwa klabu kubwa Afrika, mchezaji anapopata nafasi ya kuichezea anakuwa anaongeza thamani katika kazi yake. Ndivyo ilivyo pia na kwangu," anasema na kuongeza:
"Kupitia klabu hiyo wachezaji wazawa na wageni wameonekana na timu nyingine za nje ya Tanzania kutokana na ushiriki wake katika michuano ya CAF, hivyo anayefanya vizuri ni rahisi kupata dili."
WACHEZAJI WENZAKE
Mchezaji huyo anasema kila mchezaji aliyecheza naye Simba amebaki katika kumbukumbu ya maisha yake, kwani waliishi kwa upendo na kushirikiana katika majukumu.
"Wengi ni marafiki zangu kama Kakolanya, Bocco ambao wameondoka tayari; Kapombe, Tshabalala yaani ni wengi nawakumbuka na wengine nawasiliana nao. Maisha ya soka hayana uadui tunaweza kukutana sehemu nyingine," anasema.