Kiongozi wa Kanisa Katoliki, Papa Francis, ambaye ameugua homa ya mapafu na mkamba kwa zaidi ya wiki tatu, ameonesha shukrani kwa wahudumu wa afya wanaomhudumia, akiwapongeza kwa huduma yao yenye huruma na upendo.
Kwa Jumapili ya nne mfululizo, Papa hakuhudhuria ibada ya baraka za kila wiki, lakini Vatican ilitoa ujumbe wake wa maandishi, akieleza hisia zake za shukrani kwa madaktari na wahudumu wa afya waliopo katika Hospitali ya Gemelli jijini Roma.
“Nikiwa hapa, ninawaza juu ya watu wengi wanaowahudumia wagonjwa,” amesema Papa Francis, akiwaita wahudumu wa afya kuwa "mwanga mdogo katika usiku wa maumivu."
Taarifa kutoka Vatican imethibitisha kuwa Papa Francis ameonesha mwitikio mzuri wa matibabu katika siku za hivi karibuni, huku akiendelea kupata nafuu.
Katika ujumbe wake, Papa Francis amesisitiza kuwa huruma na utu wa wahudumu wa afya ni baraka kubwa kwa wagonjwa, akisema, "Tunahitaji huu - muujiza wa wema - ambao wale walio katika dhiki wanauhitaji."
Amehitimisha kwa kueleza kuwa huduma za kitabibu zinapochanganywa na upendo na huruma, huwa faraja kubwa kwa wagonjwa na kuwasaidia kuvumilia changamoto za afya wanazokabiliana nazo.