Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) limeufungia kwa muda Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam kutokana na eneo la kuchezea (pitch) kuendelea kupungua ubora wake.
CAF imeelekeza eneo hilo liboreshwe haraka kufikia viwango vinavyotakiwa ili kuepuka Uwanja huo kufungiwa kwa muda mrefu.
Mechi ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho la CAF (CAF CC) kati ya Simba na Al Masry ya Misri imepangwa kuchezwa kwenye uwanja huo Aprili 9, 2025.
Ili kuondoa usumbufu, Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limetakiwa kutuma jina la uwanja mbadala utakaotumiwa na Simba kufikia Machi 14, 2025.
CAF itafanya ukaguzi wa Uwanja wa Benjamin Mkapa, Machi 20, 2025 ili kuona maboresho yaliyofanyika kabla ya kuamua kuuruhusu utumike au kuendelea kuufungia.
Mbali ya mechi hizo za CAF CC, Uwanja wa Benjamin Mkapa umepangwa kutumika kwa ajili ya Fanali za CHAN zitakazofanyika Agosti 2025.