Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Christian Makonda, amewataka Wanasheria na Mawakili wanaotekeleza Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia kuwasilisha majina ya watendaji na viongozi wanaotajwa na wananchi kuwa chanzo cha migogoro ya kijamii ili hatua zichukuliwe.
Akizungumza Ijumaa Machi 28, 2025, katika Uwanja wa Ngarenaro jijini Arusha, Makonda amesema kuwa migogoro mingi inasababishwa na viongozi wazembe, wabadhirifu, wavivu, na wala rushwa, hivyo ni muhimu kuwawajibisha.
Aidha, amewataka Wakurugenzi wa Halmashauri na Wakuu wa Wilaya za Arusha kuhakikisha wanatekeleza maamuzi yatakayofikiwa kupitia kampeni hiyo, huku akisisitiza kuwa wanasheria wanapaswa kuwasikiliza wananchi kwa unyenyekevu na kufuata maadili ya taaluma zao.
Pia ameliagiza Jeshi la Polisi, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), na wakuu wa idara mbalimbali kushirikiana kikamilifu na wanasheria katika kufanikisha kampeni hiyo, kwa kuhakikisha wahusika wa mashauri wanapatikana kwa wakati.