Saa chache mara baada ya bodi ya ligi kutangaza majina ya waamuzi watakaochezesha mchezo ujao wa dabi ya kariakoo itakayopigwa jumamosi ya tarehe 8 Machi, katika dimba la Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam, mashabiki wametoa maoni yao juu ya uteuzi wa waamuzi hao.
Kwa taarifa iliyotolewa siku ya leo Jumatano tarehe 8 Machi, inaeleza kwamba waamuzi watakaochezesha mchezo huo ni Ahmed Arajiga kutoka mkoani Manyara ambaye atakua ni mwamuzi wa kati akisaidiana na washika vibendele wawili ambao ni Mohamed Mkono (Tanga) na Kasim Mpanga kutoka Jijini Dar es Salaam.
Saa chache mara baada ya kutolewa kwa taarifa hii, mashabiki na wadau mbalimbali wa soka nchini Tanzania wameonyeshwa kutoridhishwa na waamuzi walioteuliwa haswa Ahmed Arajiga ambaye amepewa dhamana ya kushika kipenga kwenye mchezo huo.
Mashabiki waliowengi wametoa mawazo yao kwamba bodi ya ligi hawana uweledi mzuri kwenye kufanya uchaguzi wa waamuzi na ndio maana mechi nyingi za hivi karibuni wamekua wakimpangia Ahmed Arajiga.
Mashabiki hao wamefika mbali sana kwa kusema kwamba ndani ya Nbc Premier league kuna waamuzi wengi wenye ubora mkubwa wa kuamua mechi hizi kubwa lakini bodi ya ligi wameamua kuwafungia vioo na kumpa kipaumbele Arajiga kwenye mechi nyingi za dabi ambazo zimepigwa kwa misimu ya hivi karibuni.
Bodi ya ligi wanatakiwa kutoa nafasi kwa waamuzi wengine ili kuwajengea uzoefu na mechi kubwa kama hizi za dabi kwa manufaa makubwa ya taifa kwa ujumla. Ahmed Arajiga amekua bora sana lakini hii haiwezi kuwa sababu ya yeye kupewa mechi nyingi za dabi kuliko waamuzi wengine.
Hoja za mashabiki hawa ziko wazi sana na zinalenga kutengeneza waamuzi bora ambao wanaweza kufikia daraja la Arajiga ili kitu ambacho kitakuwa ni faida kubwa kwa taifa la kesho haswa kwenye suala zima la mpira wa miguu.
Je, kutokana na maoni haya ya mashabiki wa soka unahisi bodi ya ligi wamefanya kitu sahihi kuwateua waamuzi hawa kuelekea kwenye dabi?.
Chanzo: Wasafi Fm, rickmediasports