Mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi wa klabu ya Simba Sc ambaye ni Rais wa heshima wa klabu hiyo Mohamed Dewji amechapisha ujumbe wake wa kwanza tangu kutokea kwa tukio la kuahirishwa kwa mchezo wa dabi ya kariakoo.
Mohamed Dewji ni tajiri wa klabu wa klabu ya Simba Sc kama ilivyokuwa kwa Ghalib Said Mohamed ambaye anawadhamini Yanga Sc kwenye mambo mengi sana ya msingi na ambayo yanahitaji pesa.
Mashabiki na wadau wa soka nchini Tanzania kwa kiasi kikubwa walikua na shauku ya kutaka kuona kwamba tajiri huyu ataongea nini mara baada ya timu yake kuonekena kwamba wamegomea mchezo wa dabi ya kariakoo siku chache zilizopita.
Mohamed Dewji ni mtu wa mitandaoni sana kwa maana kwamba amezoeleka kuwa na utamaduni wa kuchapisha taarifa na mambo mengi sana yanayohusiana Simba Sc na ndio maana wadau wengi walikuwa wanasubiri kuona kama atasema kuhusiana na sakata hilo.
Siku ya leo Jumanne tarehe 11 Machi, Mohamed Dewji kupitia kwenye ukurasa wake wa Instagram amechapisha ujumbe unaoeleza kwamba "forward we go, Simba nguvu moja", akiwa na maana kwamba "tunasonge mbele, Simba nguvu moja".
Ujumbe huu kutoka kwa Mo Dewji umetafsiriwa kuwa na lengo la kuwaweka pamoja mashabiki na wadau wa klabu ya Simba Sc ambao kwa namna moja ama nyingine walipata athari mbaya kutokana na kuahirishwa kwa mchezo wa dabi ya kariakoo.
Mashabiki wanapaswa kuendeleza mshikamano wao kama ilivyo kwa miaka yote, wanapaswa kusahau yaliyopita na kuganga yajayo ambapo Simba Sc bado anaonekana kuwa na safari ngumu ya kutaka kushinda mataji yaliyoko mbele yake kama vile Nbc Premier league, kombe la shirikisho barani Afrika pamoja CRDB Federation Cup.
Chanzo: ukurasa wa Instagram wa Mohamed Dewji.