Mwanaharakati huru, Cyprian Musiba, amemtaka Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), @tanfootball Wallace Karia, kuwaomba radhi Watanzania kutokana na kauli zake alizozitaja kuwa ni "matusi" na zisizoendana na maadili ya uongozi.
Akizungumza na Jambo TV leo, Machi 19, 2025, jijini Dodoma, Musiba amesema anashangazwa na jinsi Karia anavyotoa matamshi yasiyo na busara, hasa baada ya kuahirishwa kwa mechi ya Yanga na Simba bila kufuata kanuni.
Ameeleza kuwa alitarajia Karia angeomba radhi badala ya kutoa kauli za kejeli, na hivyo kuwataka wahusika, hususan Wizara ya Michezo, kuingilia kati suala hilo.
"Moja ya kauli zisizofaa kwa kiongozi ni kusema 'ni vitu vya kitoto na vya kijinga.' Alikuwa anamjibu nani? Unapokuwa kiongozi, hata kama una upande, ni lazima uwaheshimu wote, kwani hata wale wasiokuwa upande wako bado ni sehemu ya uongozi wako," amesema Musiba.